Events Centre
Events Available
Maonesho ya Vyuo vya Elimu Juu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ( TCU) Julai 2022
Maonesho ya Vyuo vya Elimu Juu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ( TCU) Julai 2022

Kwenye Maonesho ya Vyuo vya Elimu Juu  yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ( TCU) katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam Makamu Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini  (IRDP) anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Provident Dimoso amesema kuwa chuo hicho kina tatua changamoto za ajira kwani kimeanzisha kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali kwa wanafunzi wote wanaosoma katika chuo hicho.

Pia amewakaribisha  wahitimu wa kidato cha nne kwa ajili ya kujiunga na masomo ya ngazi ya cheti na waliomaliza kidato cha sita kujiunga ngazi ya  Shahada 'degree' pamoja na  wale ambao ufaulu wao  ni wa alama moja ' Principal Pass'  nao wanaweza kujiunga na chuo hicho kwa ngazi ya diploma.

" Imekuwa ni utamaduni kwa Watanzania kudhani kwamba ukimaliza kidato cha sita na ukapata alama moja ya ufaulu wanadhani wamefeli mwanafunzi anaweza kuendelea na masomo kwa kusoma masomo ya diploma ya chuo hiki," amesema Prof. Dimoso.

Prof. Dimoso ameongeza  chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kinatambuliwa na TCU  na kina usajili wa Baraza la elimu na mafunzo ya ufundi (NACTEVET), hivyo mwanafunzi anaposoma Shahada katika chuo hicho uzito wake ni sawa na kusoma chuo chochote duniani kwa kuwa ni kizuri,kina ubora na kimejikita kwenye masuala ya mipango.

KUPANGA NI KUCHAGUA

Read More
Serikali ya Marekani yawajengea uwezo Wanawake Wajasiriamali kukua Kiuchumi Nchini Tanzania

Serikali ya Marekani  kupitia Programu yake ya  Academy for Women Entrepreneurs (AWE) kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) imeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake wajasiliamali ili kukua kiuchumi kwa kuwawezesha kutengeneza Mpango wa biashara zao, jinsi ya kukuza mitaji na kuwaunganisha kimtandao na wafanyabiashara waliofanikiwa.

Akizungumza wakati wa Mahafali ya mafunzo hayo yaliyofanyika  Jumatatu tarehe 6, Juni, 2022 Chuoni Mipango. Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Jabiri Shekimweri  aliishukuru Serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wao nchini Tanzania kwa kuendesha mafunzo hayo muhimu na kuwashauri wanawake hao kuendelea kuchangamkia fursa zinazojitokeza ili kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Dkt. Donald Wright aliwapongeza wahitimu hao  kwa kumaliza mafunzo hayo, na kuushukuru Uongozi na Menejimenti ya Chuo cha Mipango  kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa  kuwa mwenyeji wa Mafunzo hayo  yaliyoanza tarehe 4 April, 2022 na kuhitimishwa tarehe 6 Juni, 2022.  Pia, alisema kuwa Ubalozi wa Marekani umeongeza kiasi cha  Dola za Marekani Laki Moja kwaajili ya kuendeleza Programu ya AWE  katika Mikoa mingine minne.

Aidha, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Hozen Mayaya katika hotuba yake alisema  Chuo cha Mipango kupitia Kituo chake cha Ujasiriamali na Ubunifu (MEI) kitaendelea kushirikiana na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kuhakikisha  mafunzo hayo yanaendelea kutolewa Jijini Dodoma na sehemu mbalimbali nchini.

"Chuo cha Mipango kinayo fahari kubwa kuwa mwenyeji wa mafunzo haya , ambapo  baadhi ya wahadhiri wetu walishiriki kuwezesha Programu hii kwa kuratibu na kubadilishana uzoefu na washiriki, pia mmoja wa wahadhiri wetu ameshiriki mafunzo haya ya AWE. Hivyo, ni matumaini yetu kuwa ujuzi na maarifa aliyoyapata  yatawanufaisha wanafunzi na Wafanyakazi wa Chuo."Alisema Prof. Mayaya.

Jumla ya Wanawake Wajasiriamali 31 kutoka Dodoma walishiriki mafunzo  na walitunukiwa Vyeti kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.

Read More
Chuo cha Mipango chatunukiwa tuzo ya utendaji bora

Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kimetunukiwa Tuzo ya Utendaji Bora  katika usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushika nafasi ya tatu Kitaifa katika eneo la Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu.

Akizungumza wakati wa hafla ya  kupokea Tuzo hiyo Chuoni Mipango Jumanne tarehe 31 Mei, 2022 Mgeni Rasmi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango Prof. Donald Mpanduji alipongeza kwa hatua hiyo kubwa na kusema  kuwa Tuzo hiyo ikawe dira na mwanga kwa wanamipango wote ili kuonyesha  ni wapi Chuo kinakwenda.

" Jambo hili ni jambo kubwa na la kujivunia, tuendelee kuchapa kazi na kuyasimamia yale yote tunayoambiwa na viongozi wetu na tufanye kazi kwa kushirikiana pia tuongeze bidii mwakani tushike namba Moja". Alisisitiza Prof. Mpanduji.

Akizungumza  kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kwaajili ya kupokea Tuzo hiyo na kuzungumza na Wafanyakazi wa Chuo cha Mipango , Mkuu wa Chuo cha Mipango Prof. Hozen Mayaya alisisitiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuendelea kuheshimu vipaji mbalimbali ambavyo watu wanavyo ili kukiwezesha Chuo kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine.

Read More
Wasomi Nchini wahimizwa kushiriki katika utunzaji wa Mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaasa wasomi kote nchini kushiriki katika Agenda ya utunzaji Mazingira ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuleta Maendeleo nchini. Hayo ameyasema Jumanne tarehe 31 Mei, 2022 Jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) alipofanya Ziara Chuoni hapo ikiwa ni katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani itakayoadhimishwa kitaifa Jijini Dodoma tarehe 5 Juni, 2022. "Tunaona 29.2% ya pato la Taifa linatokana na kilimo hivyo ukame ukishamiri kilimo hakitafanya vizuri na uchumi wa nchi utakua hatarini kwa hiyo tunakila sababu ya kutunza Mazingira yetu." Alisema Dkt. Jafo.

Katika Ziara hiyo Mhe. Dkt. Jafo alitembelea maeneo mbalimbali ya Chuo, kuona shughuli za uhifadhi na usafi wa Mazingira , kuona mradi wa usimamizi wa taka ngumu , mradi wa kuvuna maji ya mvua na kushiriki upandaji wa miti Chuoni hapo na kukipongeza Chuo cha Mipango  kwa kuwa na Klabu ya Mazingira inayo shiriki katika ajenda ya utunzaji wa Mazingira.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango Prof. Donald Mpanduji wakati akizungumza kabla ya Mhe. Dkt. Jafo kuongea na Jumuiya ya Chuo cha Mipango alisema kuwa Chuo kimejikita sana kufanya shughuli za Mazingira na kina wataalamu wa kutosha wa Mazingira. "Tunaomba Serikali iwatumie wataalamu wetu wa Mazingira ipasavyo kila panapokua na fursa kwani Chuo kina wataalamu wakutosha". Alisema Prof. Mpanduji.

Aidha ,  Mkuu wa Chuo cha Mipango Prof. Hozen Mayaya wakati akitoa maelezo mafupi kwa Mhe. Dkt Jafo alisema Chuo cha Mipango kinaendelea kutumia elimu, utaalamu  wa mipango katika kuhamasisha Jamii kushiriki Sensa tarehe 23 Agosti,2022.

" Tunatambua shughuli za Mazingira zitakuwa na manufaa zaidi endapo watanzania wote tutajitokeza kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi mwaka huu 2022". Alisisitiza Prof. Mayaya

Read More
Mafunzo ya Akili hisia katika Uongozi ( Emotional Intelligence in Leadership)

Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini na Viongozi wengine wa Chuo leo Alhamisi tarehe 26/5/2022 wamepata mafunzo ya siku moja juu ya  Akili hisia katika Uongozi ( Emotional Intelligence in Leadership) .

Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo  Hoteli ya Nashera Jijini Dodoma. Mwezeshaji katika Semina hiyo alikuwa Dkt. Lusajo Kajula kutoka Taasisi ya Uongozi. Aidha Semina hii itaendelea katika Vikao vijavyo vya Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini.

Read More
Vikao vya Kamati za Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP)

Wenyeviti CPA , Dkt. Samwel Werema ( Kamati ya Ukaguzi), Prof . Donald Gregory Mpanduji( Kamati ya Taaluma) na Bw. Michael John ( Kamati ya Fedha)  wakijadili mambo mbalimbali yanayogusa maendeleo ya taaluma , ujenzi wa miundombinu pamoja na maendeleo ya wafanyakazi katika Vikao vya Kamati za Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) vilivyofanyika tarehe 24/5/2022 na tarehe 25/5/2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Kampasi ya Dodoma.

Vikao hivyo vitahitimishwa na Kikao cha Baraza la Uongozi wa Chuo siku ya Ijumaa tarehe 27/05/2022.

Read More
Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) 2022

Wabunifu na Wajasiriamali ambao ni Wanafunzi na Wahitimu wa Kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali cha Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) wakionesha bunifu na bidhaa zao za kijasiriamali katika maonesho ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) mwaka 2022.

Read More
Tanzania Census 2022