Serikali ya Marekani kupitia Programu yake ya Academy for Women Entrepreneurs (AWE) kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) imeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake wajasiliamali ili kukua kiuchumi kwa kuwawezesha kutengeneza Mpango wa biashara zao, jinsi ya kukuza mitaji na kuwaunganisha kimtandao na wafanyabiashara waliofanikiwa.
Akizungumza wakati wa Mahafali ya mafunzo hayo yaliyofanyika Jumatatu tarehe 6, Juni, 2022 Chuoni Mipango. Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Jabiri Shekimweri aliishukuru Serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wao nchini Tanzania kwa kuendesha mafunzo hayo muhimu na kuwashauri wanawake hao kuendelea kuchangamkia fursa zinazojitokeza ili kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Dkt. Donald Wright aliwapongeza wahitimu hao kwa kumaliza mafunzo hayo, na kuushukuru Uongozi na Menejimenti ya Chuo cha Mipango kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 4 April, 2022 na kuhitimishwa tarehe 6 Juni, 2022. Pia, alisema kuwa Ubalozi wa Marekani umeongeza kiasi cha Dola za Marekani Laki Moja kwaajili ya kuendeleza Programu ya AWE katika Mikoa mingine minne.
Aidha, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Hozen Mayaya katika hotuba yake alisema Chuo cha Mipango kupitia Kituo chake cha Ujasiriamali na Ubunifu (MEI) kitaendelea kushirikiana na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kuhakikisha mafunzo hayo yanaendelea kutolewa Jijini Dodoma na sehemu mbalimbali nchini.
"Chuo cha Mipango kinayo fahari kubwa kuwa mwenyeji wa mafunzo haya , ambapo baadhi ya wahadhiri wetu walishiriki kuwezesha Programu hii kwa kuratibu na kubadilishana uzoefu na washiriki, pia mmoja wa wahadhiri wetu ameshiriki mafunzo haya ya AWE. Hivyo, ni matumaini yetu kuwa ujuzi na maarifa aliyoyapata yatawanufaisha wanafunzi na Wafanyakazi wa Chuo."Alisema Prof. Mayaya.
Jumla ya Wanawake Wajasiriamali 31 kutoka Dodoma walishiriki mafunzo na walitunukiwa Vyeti kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.