Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Hozen Mayaya amewaasa wanamichezo wa Chuo hicho wanaoshiriki SHIMMUTA 2023 inayoendelea Jijini Dodoma kuendelea kujituma katika kufanya mazoezi kwani mazoezi ni msingi wa ushindi. Aliyasema hayo alipokutana na wachezaji wa Chuo mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Timu za wanawake za Mpira wa Pete kati ya IRDP na WCF ambapo katika mechi hiyo timu ya IRDP ilipata ushindi mnono wa magoli 35 dhidi ya 17 ya WCF mechi iliyochezwa jana jioni katika Viwanja vya Jamhuri.
" Niwapongeze wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete kwa ushindi huu tulioupata na niwatie moyo wanamichezo wote hata katika mechi zingine zijazo muendelee kufanya vizuri ili kuiletea heshima Taasisi yetu na pia kuitangaza vizuri". Alisema Prof. Mayaya na kusisitiza " kufanya mazoezi kwa bidii na kuwasilikiza walimu wenu ndiyo msingi wa ushindi. Na inapotokea tumefungwa tusinung'unike kwa sababu kufungwa ni sehemu ya mchezo na pia ni sehemu ya kujifunza , cha muhimu ni kujua tulipokosea na kuparekebisha na kuendelea kufanya vizuri". Aliongeza Prof. Mayaya
Awali akimkaribisha Mkuu wa Chuo kuongea na wanamichezo, Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa Chuo cha Mipango Bi.Visensia Kagombora alimweleza Mkuu wa Chuo kuwa kambi inaendelea vizuri na kwamba wamejidhatiti kufuata taratibu, Sheria , kanuni za mashindano hayo.
"Ninapenda kukutaarifu kuwa wachezaji wanatambua kuwa wako kazini na kwamba wameahidi kuzingatia Kanuni, sheria, na taratibu zote za Utumishi wa Umma na za mashindano haya.", Alieleza Bi. Visensia Kagombora.