Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijjni Prof. Martha Qorro, Leo Agosti 19, 2022 ameongoza kikao cha 126 Cha Baraza la Uongozi wa Chuo kilichofanyika katika ukumbi wa Maktaba, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza.
Pamoja na mambo mengine Baraza limepokea na kujadili tathinimi ya utendaji kazi ya watumishi (OPRAS) kwa mwaka 2021/22; Limewathibitisha Wakuu wa vitengo wawili na limeridhia kubadili kada kwa watumishi wawili. Vilevile limepokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa miundo mbinu kwa Kampasi za Dodoma na Mwanza; Limejadili Rasimu ya Sera ya Usimamizi wa Miliki; Limepitisha Mpango wa Ununuzi wa Vifaa, Ujenzi na Huduma zisizo za Ushauri; na kupitisha Mpango Kazi wa Kamati zake za Taaluma; Mipango, Fedha, Ajira na Maendeleo ya Wafanyakazi; na Kamati ya Ukaguzi.
Kikao hicho cha Baraza la Uongozi kilitanguliwa na vikao vya kamati za Baraza. Siku ya Jumanne Agosti 16, 2022 kilifanyika kikao kimoja cha Kamati ya Ukaguzi kikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati CPA. Dkt. Samwel Werema. Aidha siku ya Jumatano Agosti 17, 2022 vilifanyika vikao viwili vya Kamati ya Taaluma na Kamati ya Fedha, Mipango, Ajira na Maendeleo ya Wafanyakazi vilivyo ongozwa na Prof. Donald Mpanduji na Wakili Grace Mfinanga mtawalia.
Katika hatua nyingine Wajumbe wa Baraza la Uongozi pamoja na Viongozi wa Juu wa Chuo walipata mafunzo ya uongozi wa rasilimali za umma. Mafunzo haya ya siku moja yalifanyika Alhamisi Agosti 18, 2022 yaliendeshwa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) mwezeshaji akiwa Bw. Paul Bilabaye ambae ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (PSPTB).
Akifunga Kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza ameipongeza Menejimenti ya Chuo kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa majukumu ya Chuo. Wakati huo huo amewahimiza Wanajumuiya wa Chuo cha Mipango kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23 na kutoa ushirikiano kwa Makarani wa Sensa. “Taarifa zitakazo patikana kwenye Sensa ni nyenzo muhimu kwa Mipango ya Maendeleo ya sasa na ya miaka mingi ijayo”. Alisema Prof. Qorro.