Single Event

Chuo cha Mipango chatunukiwa tuzo ya utendaji bora

Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kimetunukiwa Tuzo ya Utendaji Bora  katika usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushika nafasi ya tatu Kitaifa katika eneo la Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu.

Akizungumza wakati wa hafla ya  kupokea Tuzo hiyo Chuoni Mipango Jumanne tarehe 31 Mei, 2022 Mgeni Rasmi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango Prof. Donald Mpanduji alipongeza kwa hatua hiyo kubwa na kusema  kuwa Tuzo hiyo ikawe dira na mwanga kwa wanamipango wote ili kuonyesha  ni wapi Chuo kinakwenda.

" Jambo hili ni jambo kubwa na la kujivunia, tuendelee kuchapa kazi na kuyasimamia yale yote tunayoambiwa na viongozi wetu na tufanye kazi kwa kushirikiana pia tuongeze bidii mwakani tushike namba Moja". Alisisitiza Prof. Mpanduji.

Akizungumza  kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kwaajili ya kupokea Tuzo hiyo na kuzungumza na Wafanyakazi wa Chuo cha Mipango , Mkuu wa Chuo cha Mipango Prof. Hozen Mayaya alisisitiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuendelea kuheshimu vipaji mbalimbali ambavyo watu wanavyo ili kukiwezesha Chuo kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine.