Single Event

Wasomi Nchini wahimizwa kushiriki katika utunzaji wa Mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaasa wasomi kote nchini kushiriki katika Agenda ya utunzaji Mazingira ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuleta Maendeleo nchini. Hayo ameyasema Jumanne tarehe 31 Mei, 2022 Jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) alipofanya Ziara Chuoni hapo ikiwa ni katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani itakayoadhimishwa kitaifa Jijini Dodoma tarehe 5 Juni, 2022. "Tunaona 29.2% ya pato la Taifa linatokana na kilimo hivyo ukame ukishamiri kilimo hakitafanya vizuri na uchumi wa nchi utakua hatarini kwa hiyo tunakila sababu ya kutunza Mazingira yetu." Alisema Dkt. Jafo.

Katika Ziara hiyo Mhe. Dkt. Jafo alitembelea maeneo mbalimbali ya Chuo, kuona shughuli za uhifadhi na usafi wa Mazingira , kuona mradi wa usimamizi wa taka ngumu , mradi wa kuvuna maji ya mvua na kushiriki upandaji wa miti Chuoni hapo na kukipongeza Chuo cha Mipango  kwa kuwa na Klabu ya Mazingira inayo shiriki katika ajenda ya utunzaji wa Mazingira.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango Prof. Donald Mpanduji wakati akizungumza kabla ya Mhe. Dkt. Jafo kuongea na Jumuiya ya Chuo cha Mipango alisema kuwa Chuo kimejikita sana kufanya shughuli za Mazingira na kina wataalamu wa kutosha wa Mazingira. "Tunaomba Serikali iwatumie wataalamu wetu wa Mazingira ipasavyo kila panapokua na fursa kwani Chuo kina wataalamu wakutosha". Alisema Prof. Mpanduji.

Aidha ,  Mkuu wa Chuo cha Mipango Prof. Hozen Mayaya wakati akitoa maelezo mafupi kwa Mhe. Dkt Jafo alisema Chuo cha Mipango kinaendelea kutumia elimu, utaalamu  wa mipango katika kuhamasisha Jamii kushiriki Sensa tarehe 23 Agosti,2022.

" Tunatambua shughuli za Mazingira zitakuwa na manufaa zaidi endapo watanzania wote tutajitokeza kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi mwaka huu 2022". Alisisitiza Prof. Mayaya