Single Event

WAHITIMU CHANGAMKIENI FURSA ZA MIKOPO SERIKALINI - DULLE

Wahitimu wanaohitimu  Vyuo mbalimbali nchini wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kuchangamkia fursa za fedha za mikopo kwa vijana, wanawake na walemavu zinazotengwa na serikali kupitia halmashauri zote hapa nchini. Wito huo umetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Fedha na Mipango Bwana . Moses Dulle wakati wa ufunguzi wa kusanyiko la Kitaaluma katika Chuo cha Mipango ambalo pamoja na mambo mengine hutumika kutoa Tuzo kwa wahadhiri na wanafunzi waliofanya vizuri katika kazi na masomo mbalimbali kwa mwaka wa 2021/22.

Bwana Dulle amesema Serikali ya Awamu ya sita imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya ajira yanayowawezesha  vijana kujiajiri wenyewe kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri zote kwa ajili ya kukopesha makundi maalumu wakiwemo vijana.

" Uamuzi huu wa Serikali ni fursa kwa wahitimu wetu ambao wengi wao ni vijana na wanachotakiwa kufanya ni kujiunga katika vikundi vyao na kuvisajili katika Halmashauri walizopo Ili waweze kupata mikopo ambayo inaweza kuwasaidia kutekeleza Miradi ambayo wamejiajiri" . alisema Bw. Dulle.

Aidha Mkurugenzi huyo aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Mipango kwa kutekeleza Miradi mbalimbali ya kuendeleza miundombinu ya Chuo na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa msaada utakaohitajika kukusainia Chuo kuboresha mazingira ya kusomea na kufanya kazi. Pia, amewataka wahitimu wa Chuo cha Mipango kuungana na  Uongozi wa Chuo katika kutekeleza Miradi ya Maendeleo kama ambavyo imekua ikifanywa na wahitimu wa vyuo vingine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango Prof. Martha Qorro aliwapongeza wahadhiri na wanafunzi wote waliofanya vizuri na kuwataka kuendelea kutumia ujuzi walionao kwaajili ya kustawisha maisha yao ya Jamii .

Awali Makamu  Mkuu wa Chuo - Taluma Prof. Provident  Dimoso akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Chuo alisema katika mwaka wa 2021/22 Chuo hicho kimepata mafanikio mengi ikiwemo ongezeko la wanafunzi waliodahiliwa , watumishi pamoja na kutekeleza Miradi ya Ujenzi wa hosteli na vyumba vya mihadhara.