MINISTRY OF FINANCE

INSTITUTE OF RURAL DEVELOPMENT PLANNING

Kupanga ni Kuchagua

Event

TUJENGE UTAMADUNI WA KUWEKEZA – Profesa Mayaya

  • 2024-05-06 14:16:59

Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen K. Mayaya amewahimiza Watumishi wa Chuo cha Mipango kujenga utamaduni wa uwekezaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya fedha.

Rai hiyo ameitoa Jumatano Machi 20, 2024 katika hafla ya kufunga mafunzo elekezi kwa watumishi wa ajira mpya na waliohamia yaliyofanyika chuoni hapo katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza.

“Tujijengee utamaduni wa kuwekeza katika kipindi hiki tukiwa bado tunanguvu kwa kuwekeza kidogo kidogo kwa kile tunachokipata ilituwe na heshima na nguvu ya kifedha baada ya kustaafu. Tusisubiri kustaafu utumishi wa umma ndipo tuanze kufanya uwekezaji” Alisema Profesa Mayaya.

Aidha, amewataka washiriki hao kutumia vizuri maarifa waliyoyapa kwenye mafunzo hayo huku wakiwekeza zaidi kwenye huduma bora kwa wateja na kudumisha mahusiano ya kiutumishi baina yao na wasimamizi wao.

Katika hatua nyingine Profesa Mayaya ameshukuru na kuwapongeza wawezeshaji kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma kwa kuendesha mafunzo hayo kwa umahiri mkubwa. "Tupelekeeni salamu zetu za shukrani na pongezi kwa uongozi wa chuo kwa utayari wao mara tunapowahitaji na kwa mafunzo bora yanayoendana na wakati". Alisema Profesa Mayaya.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo haya kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC - Tabora) Bwana Richard Manase ameushukuru uongozi wa chuo kwa kuwezesha mafunzo hayo kwa watumishi na kuwakaribisha kupata ujuzi zaidi wa jinsi ya kufanya vizuri katika utumishi wa umma.

Mafunzo haya yaliyofungwa leo na Mkuu wa Chuo yamejumuisha jumla ya washiriki 53 kwa Kampasi zote mbili , Kampasi Kuu - Dodoma na Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa - Mwanza.

Subcribe weekly newsletter