Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya amewataka watumishi wa Chuo hicho kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma.
Kauli hiyo ameitoa jana Alhamisi tarehe 15 Januari alipokuwa akizungumza na watumishi wote wa Kampasi Kuu - Dodoma katika hafla ya kuuaga mwaka 2025 na kuukaribisha Mwaka 2026.
Pia Profesa Mayaya amewataka watumishi hao kupendana na kudumisha ushirikiano kazini huku wakiwekeza zaidi kwenye kutoa huduma bora kwa wadau wa ndani na nje ya Taasisi. Kipaumbele kingine ni kuwekeza kwenye tafiti bunifu ambapo ameahidi wahadhiri watapata mafunzo mbalimbali ya muda mfupi juu ya uandishi wa maandiko na tafiti shindani. Katika eneo hili amewahimiza ushirikiano baina ya watafiti wakongwe na wachanga.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Chuo amebainisha vipaumbe vya mwaka 2026 kuwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa miundo mbinu, ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa, na uhuishaji wa mitaala na kuanzisha mitaala mipya inayokidhi soko la ndani na nje.
Katika adhima ya umataifaishaji wa Chuo, Chuo cha Mipango kimeanzisha dawati la umataifaishaji ambalo hadi sasa limewezesha Chuo kuingia makubaliano ya ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi. “Ninafuraha kuwataarifu kuwa tumefikia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Eswatini, Taasisi ya "Water 4 Mercy" pamoja na Ubalozi wa Marekani,” alisema Profesa Mayaya.
Aidha, Prof. Mayaya ametumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi waliohitimu mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Shahada za Awali, Umahiri, na Uzamivu wapatao kumi na na tisa (19) waliohitimu mwaka 2025/26.
Amebainisha kuwa Chuo kitaendelea kuwezesha watumishi kupata fursa mbalimbali za elimu kwa ajili ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taasisi kwa ujumla.
Chuo cha Mipango kimekuwa na utaratibu wa kufanya mikutano hii mwanzoni mwa mwaka kwa lengo la kujadili masuala ya maendeleo ya Chuo na ustawi wa watumishi na kupeana mrejesho baina ya Menejimenti na watumishi.
Daima tunasema, Kupanga ni Kuchagua.
Register Now