MINISTRY OF FINANCE

INSTITUTE OF RURAL DEVELOPMENT PLANNING

Kupanga ni Kuchagua

Event

CHUO CHA MIPANGO KUENDELEZA JUHUDI ZA USTAWI WA MNYORORO WA THAMANI WA ZAO LA MWANI – Prof. Nkonoki

  • 2025-08-13 12:59:24

Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Juvenal Nkonoki amesema kuwa Chuo cha Mipango kupitia huduma za ushauri elekezi katika jamii kinaendeleza juhudi kubwa za ustawi wa mnyororo wa thamani wa zao la mwani nchini kwa umahili mkubwa.

 

Rai, hiyo ameitoa Jumatatu Agosti 11, 2025 alipotembelea kambi ya mafunzo ya vikundi vya wakulima wa zao la mwani vya wanawake na vijana inayoendelea katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga.

 

“Ni dhamira ya chuo kuona wakulima wa zao la mwani mnapata manufaa makubwa ya kiuchumi kupitia zao la mwani hapa nchini kwa kuhakikisha mnyororo wa thamani wa zao hili unaongezeka kupitia mafunzo mbali mbali tunayoendelea kuyaratibu kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo, hivyo tunaahidi kuendelea kusimamia mafunzo haya elekezi kwa weledi na umahili wa hali ya juu kuhakikisha tunafikia malengo”. Alisema Prof. Nkonoki.

 

Aidha, amewataka washiriki hao kuendelea kuzingatia mafunzo hayo elekezi kwa umakini mkubwa ili baada ya mafunzo haya wakawe wakufunzi wa wakulima wengine ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.

 

Mafunzo hayo ya kuvijengea uwezo wa kilimo bora, usimamizi wa vikundi, usimamizi wa fedha,utunzaji kumbukumbu, kuongeza mnyororo wa  thamani wa mazao pamoja na masoko ya zao la mwani kwa vikundi vya wanawake na vijana vya wakulima wa zao la mwani wa Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga yanayoratibiwa na Chuo cha Mipango kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa ufadhili wa Serikali ya Japan pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), yalifunguliwa Jumatatu Agosti 04, 2025 na  Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Brigedia Jenerali Hosea Ndagala na yanatarajiwa kufungwa Ijumaa Agosti 15, 2025.

Subcribe weekly newsletter
Apply Now