MINISTRY OF FINANCE

INSTITUTE OF RURAL DEVELOPMENT PLANNING

Kupanga ni Kuchagua

Event

''MIPANGO YAWAFUNDA CHAMWINO''

  • 2024-05-16 15:48:40


Na Mariam Mayunga

Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (MISO) Kampasi Kuu Dodoma mwishoni mwa wiki ilifanya ziara ya kutembelea Shule ya Sekondari Chamwino na Msanga kwa lengo la kuwapa mbinu za kukabiliana na Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia,

Akiongea na Mwandishi wa habari Makamu wa Raisi wa Serikali ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (MISO) Kampasi kuu - Dodoma Bi. Samia Musa Mohamed alisema "Tunajua Wanafunzi wa Sekondari na jamii nzima wanatambua uwepo wa Vitendo vya Kikatili vya kijinsia. Hata hivyo, tunaona kujua ni jambo moja na kuwa na mbinu za kukabiliana na Vitendo hivyo ni jambo jingine.

Hivyo tumekuja kuwapa mbinu za namna ya kukabiliana na Vitendo vya Ukatili wa kijinsia katika mazingira mbalimbali," alisema na kuongeza Vilevile tumelenga kuwajengea ujasiri katika kukabiliana na kuripoti vitendo hivyo vya ukatili wa Kijinsia.

Viongozi hao wa MISO vilevile walitumia ziara hiyo kutoa msaada wa madaftari, kalamu, taulo za kike na za watoto kwa Wanafunzi hao wakiwemo wanafunzi wa Programu ya Mama Samia.

Programu ya Mama Samia ni programu ya wanafunzi waliopata mimba wakiwa Sekondari na hivyo kuruhusiwa kurudi shuleni na kuendelea na masomo.

Kwa nyakati tofauti wanafunzi wanaonufaika na programu ya Mama Samia wanaosoma Chamwino Sekondari wameishukuru Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Mipango (MISO) kwa msaada wa vifaa na eimu ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Wakati huohuo Mkuu wa Shule ya Sekondari Chamwino Mwalimu Dominic Thomas Sullumo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa iliyofanya katika sekta ya elimu hapa nchini ambapo shule za Sekondari sasa zina mazingira bora na wezeshi katika tendo la kujifunza na kufundishia.

"Hivyo, ninawaasa wazazi na walezi kuwasimamia wanafunzi kuhudhuria shuleni na sisi tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa katika kutimiza wajibu wetu" alisema Bwana Dominick Sullumo.

Kupanga ni Kuchagua#

Subcribe weekly newsletter