Event

WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU WATAKIWA KUWA NA WIVU NA NCHI YAO

  • 2025-12-01 12:49:34

WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU WATAKIWA KUWA NA WIVU NA NCHI YAO

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Magu ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Magu Mheshimiwa  Jubilate Lawuo amewataka wanafunzi wa elimu ya juu nchi kuwa na wivu na nchi yao ya Tanzania.

Rai hiyo ameitoa Ijumaa Novemba 29, 2025 katika kikao cha Kamati ya  Usalama wilaya ya Magu na Wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini , Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza kilichofanyika kituoni hapo Kisesa  Wilayani Magu.

“Jukumu la amani katika nchi yetu ni letu sote . Tukumbuke tangu kupata Uhuru wa Tanganyika na Uhuru wa Zanzibar kupitia Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na kisha kupata Muungano wa Tanzania  tumeishi maisha yetu yote  kwa amani.  Hivyo, ninyi vijana mnasababu ya kila aina  kuilinda na  kuihubiri  amani kama walivyofanya wazazi wetu  walipo kuwa vijana. Ilikuilinda amani ya nchi yetu  tunapaswa kuwa na wivu na nchi yetu ya Tanzania kwa kuwa wazalendo. Tuijenge  Tanzania ijayo yenye mafanikio makubwa kwa uongozi thabiti wa Mheshiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani”. Alisema Mhe.  Lawuo.

Aidha, Mheshimiwa Lawuo amewahakikishi Wanafunzi hao kuwa Wilaya ya Magu ipo salama hivyo katika kipindi hiki cha masomo waendelee na ratiba za masomo kama zilivyopangwa na Chuo kwa kuweka juhudi na bidii katika masomo yao kwa kufuata taratibu na miongozo inayotolewa  na serikali na kujiepusha na makundi yasiyo kuwa na mwenendo mzuri.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bw. Mohamed Ramadhani amewahakikishia Wanajumuiya wote wa Chuo cha Mipango, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa - Mwanza kuwa huduma zote katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu zinaendelea kutolewa kwa ufanisi mkubwa hivyo kama kuna changamoto ya aina yoyote ofisi yake na watendaji wake milango yao ipo wazi kutatua changamoto hizo kwa wakati.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Dkt. Ezekieli Kanile ameishukuru Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Magu ikiongonzwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Magu Mheshimiwa Lawuo kwa kukitembelea Kituo na kuzungumza na Wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo kwa Mwaka wa Masomo 2025/26. Vilele , amesema kuwa Kituo kitaendelea kushirikiana na Serikali ya Wilaya na Mkoa  kwa kufuata miongozo na maelekezo yanayotolewa na serikali.

Subcribe weekly newsletter
Register Now