CHUO CHA MIPANGO CHAPONGEZWA KWA KUIUNGA MKONO SERIKALI KATIKA HUDUMA ZA JAMII MAGU
Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kimepongezwa kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo hususani huduma za jamii wilayani Magu.
Pongezi hizo zimetolewa na Mbuge wa Jimbo la Magu Mheshimiwa Boniventure Destery Kiswaga (Mb) katika hafla ya uzinduzi wa Zahanati ya Chuo, Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, pamoja na uzinduzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kitumba, Kata ya Kisesa Wilayani Magu.
“Naomba nitumie fursa hii kuupongeza uongozi wa Chuo cha Mipango kwa namna ya kipekee kwani tangu kuhamia hapa mwaka 2021 mmekuwa sehemu muhimu ya wanajumuiya wa kata ya Kisesa na wilaya ya Magu kwa ujumla kwani tumeshuhudia mabadiliko makubwa kiuchumi katika eneo letu”, alisema Mhe. Kiswaga, nakuongeza "mmekuwa wadau wetu katika elimu, afya na mambo mengine ya kimaendeleo. Aidha, tunawashukuru sana kwa mchango wenu na ushirikiano kwa wananchi katika kukamilisha Zahanati ya Kijiji hiki cha Kitumba niliyoifungua hivi punde pia nawapongeza viongozi wa chuo kwa kukamilisha zahanati ya kituo chenu ambayo pia niliifungua mapema hii leo zahanati inakwenda kuhudumia siyo tu wanafunzi peke yao bali pia itahudumia wananchi wanaozunguka kituo chetu". Alisema Mhe. Kiswaga.
Mheshimiwa Kiswaga amesema mchango wa chuo wa ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kitumba vyenye thamanj ya zaidi ya shilingi milioni 17 pamoja na mchango wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mondo wilayani humo ni kielelezo cha utekelezaji kwa vitendo wa dhana ya maendeleo vijijini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa- Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Juvenal Nkonoki amesema Chuo kitaendelea kuunga mkono juhudi za serikali na wananchi katika kuboresha huduma za jamii.
Profesa Nkonoki ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Wilaya ya Magu kwa kuleta wahudumu wa afya na vifaa tiba vya kuanzia kwa ajili ya kutumika katika Zahanati ya Chuo.
Vilevile, Prof. Nkonoki amemshukuru Mbuge wa Jimbo la Magu Mheshimiwa Kiswaga kwa kukubali ombi la kuzindua Zahanati ya Kituo iliyogharimu jumla ya shilingi milioni 135.