Event

MIPANGO WAKO TAYARI KUSHIRIKIANA NA TAASISI MBALIMBALI KWA MAENDELEO ENDELEVU

  • 2025-12-22 09:57:38

Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) umeeleza utayari wake wa kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuimarisha elimu, utafiti na maendeleo endelevu ya Taifa.

Kauli hiyo ilitolewa tarehe 19 Desemba 2025 na Dkt. Africanus Sarwatt wakati akihitimisha rasmi mafunzo ya muda mfupi ya ujenzi wa uwezo, yaliyofanyika mkoani Morogoro, kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Sarwatt alisema kuanzia mwaka wa masomo 2025/26 Chuo kitaanza kuendesha kozi kwa mfumo wa "hybrid blended learning" unaochanganya masomo ya ana kwa ana na mtandaoni, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa elimu kwa wadau mbalimbali hususan wale wenye majukumu ya kikazi yanayowazuia kuhudhuria masomo ya kawaida.

Alieleza kuwa uanzishwaji wa mfumo huo umetokana na maombi ya muda mrefu kutoka kwa wadau wa Chuo, na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Chuo katika kuboresha utoaji wa elimu na kuendana na mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya soko la ajira.

Dkt. Sarwatt aliwahimiza washiriki wa mafunzo hayo pamoja na taasisi nyingine kuendelea kushirikiana na Chuo katika masuala ya kitaaluma, utafiti na ujenzi wa uwezo, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya taasisi na Taifa kwa ujumla.

 

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yameleta matokeo chanya kwa kuongeza maarifa na ujuzi wa washiriki, sambamba na kuimarisha mtandao wa ushirikiano kati ya Chuo na wadau wake kutoka sekta mbalimbali.

Jumla ya washiriki 110 wamenufaika na mafunzo hayo ya muda mfupi.

Kwa upande wake, Dkt. Titus Mwageni, akizungumza kwa niaba ya wawezeshaji, aliishukuru taasisi shiriki kwa kuchagua Chuo cha Mipango kuwa taasisi ya kuwajengea uwezo, na kuahidi kuwa wataendelea kuandaa mafunzo mafupi yanayojibu changamoto za kiutendaji na maendeleo kulingana na mahitaji ya wadau, kwa manufaa mapana ya Taifa.

Subcribe weekly newsletter
Register Now